Back to School Project 2017 by Flaviana Matata Foundation

Taasisi ya Flaviana Matata Foundation (FMF) leo imezindua rasmi msimu wa muhula/mwaka mpya wa wa masomo 2017 #BackToSchool2017 kwa kutoa msaada wa vifaa vya kujifunzia kwa wanafunzi 317 wanaosoma Shule ya Msingi Msinune iliyopo kata ya Kiwanga wilayani Bagamoyo mkoani Pwani. Msaada huo umekabidhiwa moja kwa moja kwa wanafunzi ikiwa ni moja ya juhudi za Taasisi kuinua kiwango cha elimu kwa kuwahamasisha wanafunzi mashuleni. Katika harakati zake za kuinua kiwango cha elimu shuleni Msinune na kurahisisha upatikanaji wake, pamoja na kugawa vifaa vya kujifunzia na kufundishia kwa wanafunzi na walimu; Taasisi ya Flaviana Matata imefanikiwa kujenga na kukarabati madarasa, kujenga vyoo kwa ajili ya walimu na wanafunzi na kutoa msaada wa madawati. Akizungumza wakati wa kupokea msaada Kaimu Mkuu wa Shule ya Msinune alisema kwamba tangu taasisi ya Flaviana Matata ianze kutoa misaada shuleni hapo kumekuwa na upungufu wa utoro kwa wanafunzi na pia idadi ya wanafunzi waliomaliza darasa saba imeongezeka kutoka 18 waliomaliza mwaka 2015 mpaka 46 kwa mwaka 2016. Pia ufaulu wa wanafunzi umeongezeka kwa asilimia 2.64; mwaka 2015 wanafunzi 5 walichaguliwa kujiunga na masomo ya sekondari na kwa 2016 wanafunzi 14 walichaguliwa. Akielezea changamoto zinazowakabili, Kaimu Mkuu wa Shule amezielezea kwamba ni pamoja na Elimu kukosa kipaumbele wilayani Bagamoyo, upungufu wa vyumba vya madarasa, uhaba wa walimu (shule ina walimu 6), ukosefu wa nyumba za walimu na mila na desturi za wakazi wa eneo hilo ambao wanafanya jitihada kuzuia watoto wa kike wasiendelee na elimu ya sekondari ili waweze kuolewa, hii hupelekea wazazi wa watoto wa kike kuwalazimisha wajifelishe wakati wa mitihani ya kumaliza darasa la saba. Akiongea wakati wa kukabidhi misaada hiyo, mwanzilishi wa Taasisi na Mlezi wa shule ya Msinune Flaviana Matata alisema kwamba Taasisi yake itaendelea kuisimamia na kujitahidi kuiboresha shule hiyo kwa kumalizia kujenga madarasa yaliyobaki na kuangalia namna ya kuwashirikisha wadau wengine wa elimu na serikali kushughulikia nyumba za walimu.
Picture and story by Flaviana Matata Foundation


xoxo
Missie Popular

0 comments:

Post a Comment